1 Sep 2010

Editorial/Tahariri: Kuweka Jamii Kwanza Hapa Njombe

Friends and followers of Daraja on Facebook and on Twitter, as well as those here in Njombe, will know that we launched our Kwanza Jamii Njombe local newspaper this week. A report on the launch, together with pictures of Mrisho Mpoto and others will be available here soon. In the meantime, as we unfortunately don't have the website for the paper up and running yet, we felt it was right to share a few articles from the first issue of the paper here on this blog. We will therefore be posting some of the best articles and features over the next few days and weeks, starting here with the first editorial.

(Apologies to readers who prefer things in English, but we also have many readers who are more comfortable in Swahili. And we will continue to post here in English as well.)


Kuweka jamii kwanza hapa Njombe


Mwitikio wa watu umekuwa mkubwa tangu pale tulipowapa wazo letu la kuanzisha gazeti la kijamii hapa Njombe. Asilimia kubwa wamefurahishwa na wazo letu, huku wakitarajia kuliona lina nini ndani yake.

Maoni mengi ambayo yalitolewa na wananchi juu ya ujio wa gazeti letu yametufikia na tumeshaanza kuyafanyia kazi katika toleo hili la kwanza. Pia, tumetoa nafasi kwa wengine katika ukurasa ufuatao kuchangia maoni yao juu ya maslahi ambayo uwepo wa gazeti unaweza kuleta kwa wakazi wa mji na wilaya ya Njombe.

Wengine wamesisitiza mchango wa gazeti kusaidia watu wajue kinachoendelea katika maeneo mbalimbali ya Njombe, kama ni shughuli za maendeleo, habari za halmashauri, biashara au hata burudani na michezo, maana binadamu huwa hatupendi kubaki gizani. Hayo yote yapo humu ndani.

Pia kuna kundi la watu waliotambua kuwa gazeti linaweza kuwa jukwaa la kuwapa watu fursa ya kuchangia mawazo yao, ili sauti yao isikike. Hivyo, humu ndani utakuta kurasa nyingi zinazobeba maoni ya jamii na mijadala.

Wengine wameliona gazeti hili kama mwalimu, litakaloelimisha jamii kuhusu maswala mbalimbali. Katika toleo hili la kwanza kuna kurasa za elimu juu ya uchaguzi. Elimu ya uraia, afya, mazingira na mengi zaidi yatafuata.

Gazeti la Kwanza Jamii Njombe ni tofauti na magazeti mengine kwa maana inayoonekana katika jina lake. Ni gazeti linaloweka jamii kwanza, na ni gazeti la Njombe.

Maana ya kuwa gazeti la Njombe ni kwamba habari zote ni za matukio ya hapa hapa ndani ya mji na wilaya ya Njombe. Hata habari za michezo na burudani ni za hapa hapa. Tuna kurasa za historia na utamaduni wa Njombe. Na maoni ni ya wakazi wa Njombe.

Maana ya kuwa gazeti la kijamii ni kwamba tunaweka kipaumbele maslahi ya wanajamii. Tunaisaidia jamii kujua kinachoendelea, uhalisia wa maendeleo, kueleza mahitaji yake, kuchangia maoni yao. Pia, tunasikiliza sana mapendekezo ya wanajamii kuhusu kazi zetu. Tuweke nini katika gazeti hili? Tuambia unachopenda kusoma, na tutajitahidi kulifanyia kazi.

Kwanza Jamii Njombe si gazeti la biashara, lenye lengo la kujipatia faida, wala si la kisiasa, lenye lengo la kupigia debe chama chochote au mwanasiasa fulani. Na siyo gazeti linaloandaliwa na chombo cha kiserikali au kanisa lolote. Bali ni gazeti huru, lenye lengo la kuisaidia jamii ya mji na wilaya ya Njombe. Twende Pamoja.