28 Sep 2010

Maji na vita ya kupigania maisha


This op-ed article was originally published today in the HakiElimu Kauli Mbadala spot in Mwananchi newspaper, Tuesday 28 September.


Maji na vita ya kupigania maisha


Siwema anakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kila siku. Anaishi kijiji cha Godegode wilayani Mpwapwa ambapo sehemu ya karibu anayoweza kupata maji safi na salama ni kijiji cha jirani kilichopo umbali wa zaidi ya kilometa tano. Kila siku Siwema ana chaguo, aidha atembee umbali mrefu kwa zaidi ya masaa mawili kwa ajili ya kupata maji safi na salama au akachote maji kwenye dimbwi lililopo kwenye mto uliokauka ambapo maji ni machafu na tayari yananuka. Kijiji cha Godegode kiliwahi kuwa na kisima kirefu cha maji lakini kiliharibika miaka michache iliyopita na hakijafanyiwa matengenezo.Ni nini kinaweza kuwa muhimu kama maji? Maisha hayawezekani bila Maji, na kwa wale ambao hawapati maji safi na salama, maisha kwao yanakuwa ni mapambano kila siku. Mapambano haya ni makubwa kiasi cha kuweza kupoteza maisha ya watu kwa magonjwa, kuongeza umasikini kwa jamii na watoto wetu kushindwa kupata elimu bora.


Lakini haya si mapya. Kwanini jitihada za pamoja za serikali ya Tanzania na wafadhili kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama hasa vijijini hazioneshi mabadiliko?


Hebu tupitie baadhi ya takwimu. Mwaka 2000, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zilionesha kuwa asilimia 46% ya kaya zilizopo vijijini nchini Tanzania zilikuwa zinapata maji safi na salama.  Mwaka 2007, takwimu kutoka ofisi hiyo zilionesha kuwa hali hiyo imeshuka hadi kufikia kaya asilimia 40% tu (takwimu kutoka Sensa ya Bajeti ya Kaya – HBS). Kuna vituo vya maji (mabomba) takriban 62,000 Tanzania vijijini, ambapo kwa nadharia vinatosha kuwapatia maji wananchi karibu milioni 20. Lakini hali halisi ya vijijini hapa Tanzania ni wananchi milioni 12 tu ndio wanaopata maji safi na salama. Hii ni kwa sababu vituo vya maji chini ya asilimia 60% vijijini ndio yanafanya kazi (Sensa ya Utambuzi wa Vituo vya Maji – WPM – ya WaterAid na GeoData). Hata baada ya miaka miwili tu, robo ya mabomba mapya yanakuwa tayari yameharibika (hayatoi maji).


Bila ya kushangaza, wananchi waishio vijijini wanapoulizwa kuhusu vipaumbele vyao kwa serikali kuwatekelezea, maji yamekuwa ni kipaumbele cha kwanza. Utafiti wa Afrobarometer wa mwaka 2008 unaonesha kuwa asilimia 44% ya wananchi wa vijijini wanasema maji ni miongoni mwa vipaumbele vyao vikuu vitatu. Vipaumbele vingine vilivyoainishwa ni barabara kwa asilimia 33%, kilimo kwa asilimia 31% na elimu kwa asilimia 15%. Katika muktadha huo huo, asilimia 39% pekee ya wananchi wa vijijini wanaridhishwa na juhudi za serikali katika kuwapatia maji, ukilinganisha na asilimia 64% ambao wanaridhishwa na juhudi za serikali kwenye afya na asilimia 80% kwenye elimu.


Kwa sasa takwimu hizi zina umri wa miaka miwili, na toka mwaka 2007 kumekuwa na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ambayo inaingiza takriban dola bilioni moja kwenye sekta ya maji. Mojawapo ya malengo ya programu hii ni kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini. Hivyo labda hali imebadilika? Ndivyo tunavyotumaini, ingawa ni vigumu kufahamu kwa uhakika hali ilivyo sasa, inabidi tusubiri kupata takwimu kutoka kwenye tafiti za karibuni zaidi.


Lakini utekelezaji wa Programu hii ya Maendeleo ya Sekta ya Maji hauendi vizuri sana. Mpango wa kufadhili miradi mipya ya maji kwa vijiji kumi kwa kila wilaya unawezekana ukasubiri kwanza kwa sababu pesa nyingi zimetumika kwenye mikataba na makampuni ya wahandisi kubuni (designing) miradi ambayo mwisho wake pesa zinakosekana za kutekeleza miradi hiyo. Pengine kutokana na upungufu huu vijiji vinne tu katika kila wilaya ndivyo vitafanikiwa kupata fedha za miradi mipya ya maji.


Na pia upatikanaji wa pesa hizo kwa ajili ya hivyo vijiji vichache sio wa uhakika. Mwanzoni mwa mwaka huu wafadhili wakubwa wamesimamisha ufadhili wa Programu hii mpaka hapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji itakapoboresha utekelezaji. Programu hii ya Maendeleo ya Sekta ya Maji sasa inafanyiwa marekebisho ili kujaribu kutatua matatizo haya. Mapendekezo ya maboresho ni pamoja na kupunguza idadi ya vijiji kwa theluthi mbili toka vijiji 1320 hadi 460 na kutaka kuhusisha zaidi mamlaka za serikali za mitaa katika utekelezaji.


Marekebisho haya yanapelekea vijiji zaidi ya theluthi mbili ambavyo tayari vilikwisha hamasishwa, kutokupata fedha kwa ajili ya miradi mipya. Kwa bahati mbaya tayari fedha zimeshatumika kwa washauri na wahandisi kubuni na kuandaa mipango kwa ajili ya vijiji kumi. Je juhudi na fedha hizi zinapotea kabisa? Ni vigezo gani vitatumika kuchagua vijiji vinne kati ya hivyo kumi? Wananchi wamehamasishwa na wamehamasika, je watalichukuliaje hili?


Kwa wakati huu ambao marekebisho yanaendelea, Siwema na wananchi wengine wanaoishi kwenye mazingira kama hayo wataendelea kuhangaika kwa ajili ya kupata maji kwa maisha yao. Kisima kilichoharibika haifahamiki hatima yake ni nini? Je akina Siwema hawafahamu wajibu na majukumu yao ya kulinda na kusimamia miradi ya maji kama sera inavyoelekeza? Je akina Siwema hawana chombo cha watumia maji kinachoweza kufanya kazi ya kufufua kisima chao?