15 Nov 2010

Wazo Tete - Maswali na majibu na Kapongola Nganyanyuka, mtafiti wa Daraja

Kapongola
Afisa Ufuatiliaji na Utafiti wetu, Kapongola Nganyanyuka, alihojiwa na Radio Uplands FM wa hapa Njombe wiki iliopita juu ya kazi za Daraja na mfumo mzima wa mipango shirikishi. Kifuatacho ni badhi ya maswali na majibu kutoka kwa kipindi hiki:

1. Nini hasa kilichopelekea mpaka kuamua kujishughulisha na programu ya kuwaleta wananchi na serikali pamoja mkoani Njombe

Ahsante sana ndugu...... Kwanza kabisa naomba nitoe utangulizi wa shirika la Daraja. Daraja ni shirika la kiraia ambalo linashughulika na utawala bora hasa katika kuleta wananchi na serikali pamoja. Dira ya Daraja ni kuona serikali za mitaa zinafanya kazi kikamilifu kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya wananchi na kutimiza wajibu wao wa kupunguza umaskini vijijini. Shirika la Daraja lina makao makuu mjini Njombe. Pia ni vizuri kufahamu kua shirika la Daraja limeanza kazi mwaka 2009, hata hivyo ofisi ya kudumu ilifunguliwa mwanzoni mwezi Januari mwaka huu.

Nikirudi katika swali lako, kuna sababu kuu tatu zilizopelekea kuanzishwa kwa Daraja. Nazo ni
  1. Msukumo mdogo kutoka kwa wananchi wa kuiwajibisha serikali ili ifanye kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya jamii
  2. Serikali kuu na wahisani bado wanazuia na kupunguza uhuru kamili wa serikali za mitaa
  3. Wananchi hawaamini uwezo wa serikali za mitaa na serikali za mitaa hazijali vipaumbele vya wananchi wao
2. Kupitia utafiti ambao mmekwisha ufanya mnaweza kuzungumzia vipi maada hii, je, wananchi wanashirikishwa ipasavyo au la?

Ni vizuri neno ipasavyo limetumika katika swali lako kwani wananchi wanashirikishwa kwa kiwango fulani, hata hivyo si kwa matarajio ya mchakato wa kupeleka madaraka karibu na wananchi.

Pia ieleweke kwamba si Daraja pekee iliyotambua ushiriki mdogo wa wananchi katika masuala yahusuyo ustawi na maendeleo yao. Serikali pia inatambua hilo, kwa mfano mada iliyoandaliwa kwa ajili ya semina ya madiwani mwaka 2006 ilieleza tatizo la ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za kimaendeleo hasa katika mipango.

Kuna njia kuu mbili za ushiriki wa wananchi katika utawala bora. Moja ni njia ya uwakilishi ambayo pia huitwa (indirect) na ya pili ni wananchi wenyewe kushiriki mmoja mmoja. Katika kuchagua wawakilishi, wananchi wanashirikishwa katika uchaguzi wa viongozi na hii ndiyo njia inayoeleweka na wengi. Hata hivyo ina mapungufu kwani mara nyingi wananchi wanakumbukwa nyakati za uchaguzi tu.

Kuna mapungufu makubwa pia katika ushiriki wa wananchi katika upangaji wa mipango ya maendeleo, utekelezaji na ufuatiliaji wa utendaji wa serikali.

Na je, kama mmegundua wananchi hawashiriki ipasavyo ni kutokana na sababu zipi?

Sababu za ushiriki mdogo wa wananchi katika kuamua ziko katika makundi makubwa mawili, upande wa mwananchi mwenyewe na pia upande wa serikali.

Kwa upande wa mwananchi, uelewa mdogo wa wajibu na majukumu ya mwananchi kushiriki katika maendeleo. Pia ukosefu wa taarifa za muundo na mienendo ya serikali na kukosa kufahamu jinsi ya njia za ushiriki.

Kwa upande wa serikali, maamuzi mengi yanafanywa na halmashauri au serikali kuu bila kwanza kupata maoni yao. Kuna utawala msonge ambapo viongozi wamegeuka kuwa mabwana wenye kutoa amri na kufuatilia utekelezaji wake kwa nguvu zote.

3. Ni mafanikio gani ambayo mmekwisha yapata tangu kuanzishwa kwa shirika hili na je ni mikakati ipi ambayo unayo kuhakikisha mnatimiza malengo yenu

Pengine ni vizuri kutofautisha mafanikio ya kiutendaji na yale yatokanayo na kazi zetu. Tukianza na mafanikio ya kazi zetu, kwa sasa ni mapema sana kutoa tathmini ya mafanikio ya kazi zetu kwani tumeanza kazi zetu hivi karibuni. Ifahamike kwamba kazi zetu ndiyo kwanza zimewafikia wananchi kwa mara ya kwanza hivi karibuni.

Hata hivyo tumepata mafanikio makubwa kwa upande wa utendaji. Suala kuu na la muhimu ni ushirikiano mzuri baina yetu na wananchi pamoja na serikali. Wananchi wamepokea kazi zetu kwa mwamko mkubwa, kwa mfano upokeaji mzuri wa gazeti letu la Kwanza Jamii. Halmashauri pia imekubali kufanya kazi nasi hasa katika programu ya Maji matone, hususani mradi wa Ujumbe mfupi wa Maandishi kupitia Simu za mkononi.

Pia tumepata wafanyakazi wenye moyo na ari ya kufanya kile Daraja ilichotarajia. Kwa bahati nzuri Daraja inaundwa na vijana wenye nguvu thabiti na uchungu wa maendeleo na nchi yao.

Hii inatushwawishi kuboresha mawasiliano na mahusiano mazuri kati yetu na wadau wengine wa utawala bora ikiwemo serikali na wananchi.

4. Katika kipeperushi chenu katika kipengele kinachoonyesha shughuli zenu, kuna kipengele kinachosema kuwezesha ufuatiliaji wa fedha za umma? Je ni kivipi mnatimiza hili?

Kwanza ningependa kukazia kwamba sisi kama wananchi ndiyo wenye jukumu la kufuatilia na kutathmini utendaji wa serikali. Daraja pia inaamini hivyo.

Baadhi ya changamoto walizonazo wananchi katika kutimiza wajibu huu ni kukosa ufahamu juu ya wajibu wa kufuatilia utendaji wa serikali, kukosa taarifa ya njia na utaratibu wa ufuatiliaji. Kwa upande mwingine, mifumo ya serikali inaweza kuleta vikwazo vya wananchi kufuatilia utendaji wake mfano, mifumo ya utoaji wa taarifa na usiri.

Hivyo Daraja itaelekeza juhudi zake katika kuwaelimisha wananchi juu ya wajibu wao katika kufuatilia utendaji wa serikali ikiwemo matumizi ya pesa za maendeleo. Hata hivyo, Daraja inafanya tafiti kutambua vikwazo vya wananchi kushiriki kimamilifu katika ufuatiliaji. Kwa kutumia matokeo ya utafiti huo, Daraja itashirikiana na serikali kwa majadiliano na ushawishi ili kuondoa vikwazo vitakavyotambuliwa.

Mfano: Toleo la kwanza la Kwanza jamii liliandika makala kuhusu uzoefu na ugumu wa mwananchi kufuatilia taarifa za kiserikali hasa zinahusiana na matumizi ya pesa. Pia toleo lijalo la kwanza Jamii linatazamia kutoa mahesabu ya mwaka ya halmashauri ya Njombe mjini. Zote hizi ni juhudi za kuwafanya wananchi wapate taarifa kuhusu matumizi ya pesa za serikali.