21 Dec 2011

Lala salama Mzee Njoo Uone

  Below is an obituary of Mzee Augustine "Njoo Uone" Hongole, inspirational journalist and activist, and Chair of Kwanza Jamii Njombe's Editorial Board. He will be much missed. This obituary, by our Managing Editor, Simon Mkina, will be published in Kwanza Jamii newspapers next week.


  Lala salama Mzee Njoo Uone
  • Nyota yake imezima ghafla, akiwa anahitajika kujenga maadili, kutetea chai
  Na Simon Mkina


  Mzee Augustino "Njoo Uone" Hongole
  DESEMBA 13, mwaka huu wa 2011 ilikuwa siku ya mwisho kabisa kuuona mwili wa Mzee Augustino Hongole maarufu kama Mzee ‘Njoo Uone’. Ni siku ambayo mwili wake ulibeba zaidi ya tani moja ya mchanga kuutenganisha na uso wa dunia hii.

  Ni siku ambayo waliompenda sana, waliompenda, waliomchukia, waliomchukia sana, watabaki na taswira ya umbile la mwanahabari huyo, aliyetumia siku zake hapa duniani, kukamilisha kazi aliyotumwa kuifanya.

  Ndiyo. Kazi aliyotumwa ameikamilisha. Sasa ameondoka na kwenda huko alikokwenda.

  Sina uhakika kama amekwenda kufanya kazi nyingine au kupumzika, kwa kuwa imani yangu juu ya majukumu ya Mungu anayompangia mwanadamu, mara zote hugota pale pumzi ya mtu inapokoma, ingawa roho yake, inatajwa na baadhi ya watu na vitabu, hupaa mbinguni. Hata hivyo, haya ni masuala ya imani zaidi.

  Yawezekana kabisa Mzee Augustino Hongole, mwandishi aliyetumia vyema nafasi ya dhamana zake, elimu na uwezo wake kuelimisha umma wa Watanzania, hasa wa maeneo ya kusini mwa Tanzania, amekwenda kufanya kazi kubwa zaidi huko alikokwenda. Pia yawezekana amekwenda kupumzika, baada ya kazi ngumu hapa juu ya uso wa dunia.

  Hata hivyo, kwa hulka na maumbile ya nafsi ya mwanadamu, siri ya kifo imefichwa na kuwa sababu kubwa ya watu kuomboleza na kulia kila mpendwa wao anapoiaga dunia.

  Tangu kusambaa kwa taarifa za kifo cha Mzee Njoo Uone, machozi ya wapendwa wake yamekuwa yakibubujika juu ya mashavu yao, wakilia kuukosa ustaarabu wake, uchangamfu uliomjaa, wema aliokuwa nao na zaidi sana namna alivyokuwa akijali matatizo ya wengine na kuyatatua pale alipoweza.

  Hongole atakumbukwa pia kwa namna alivyotumia kipaji chake kukemea, hata kuchapa wakati mwingine, kwa wote walioonekana kwenda kinyume na maadili ya Tanzania.

  Mzee huyo alikuwa mkali kweli kweli kwa wasichana waliokuwa wakivaa nguo fupi, suruali zinazobana na wale wanaopenda kuvaa nguo zikionesha maziwa yao.

  Kila alipokutana nao, iwe barabarani, ndani ya vyombo vya usafiri na hata ofisi alizokuwa akizitembelea, hakusita kufungua kinywa chake kukemea na wakati mwingine kutumia bakora inapolazimu kufanya hivyo.

  Hakufanya hivyo kwa kuwa labda alikuwa hapendi wasichana, la hasha. Hata kwa wavulana waliokuwa wakivaa suruali zao mapajani na kuacha nguo zao za ndani zikionekana, hakusita kuwacharaza bakora, bila kujali anawajua au hawajui.

  Ni kutokana na kupenda maendeleo ya watu, kutetea wanyonge na zaidi sana kulinda maadili na staha ya Mtanzania, Mzee Hongole alifahamika kila pande za Iringa, Morogoro na sana mkoa mpya wa Njombe.

  Alikuwa akiishi katika Kijiji cha Isoliwaya katika tarafa ya Lupembe ambako aliamua kuweka makazi huko baada ya kustaafu utumishi. Akiwa kijijini Hongole alisimamia mashamba yake ya chai na mazao mengine, huku akichaguliwa kuwa mtetezi mkuu wa wakulima wa chai wa tarafa ya Lupembe na maeneo jirani.

  Wengi waliowahi kufanya kazi na Mzee Augustino Hongole, wanatambua haiba aliyokuwa nayo mwanahabari huyu kwa kila mtu bila kujali umri, cheo, uwezo wa elimu wala fedha na namna alivyokuwa akijitoa kusaidia wengine.

  Mzee Augustino Hongole ambaye wengi walizoea kumwita kwa majina tofauti tofauti, kulingana na wakati na mahali, wanatambua namna alivyokuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya watu aliokuwa akiwaongoza.

  Nakumbuka pia namna Mzee huyu alivyokuwa akisikitishwa na ujira mdogo, waliokuwa wakipata baadhi ya waandishi katika vikao vya wahariri vya ndani ya vyumba vya habari, alivyowahi kuvifanyia kazi au kwenye mikutano ya kujadili mustakabali wa tasnia ya habari nchini.

  Mzee Hongole alikuwa na ndoto kwamba waandishi wa habari, kama inavyopaswa kuwa kwa wanataaluma adhimu; walimu na madaktari, walipwe zaidi ya wanasiasa ambao kazi yao kubwa ni kupiga domo majukwaani.

  Aliwahi kunieleza, siyo mara moja wala mbili, namna alivyokuwa akichukia kuona wanasiasa wamenona, kwa malipo makubwa ya mishahara na marupurupu, huku walimu au madaktari wakipanga kila namna ya kugoma kuongezwa ama kulipwa mishahara yao kwa wakati.

  Mara zote alipotokea mwanasiasa, hakusita kutamka wazi- “Simon hebu ona huyu alivyonona kwa kodi zetu, lakini walimu waliomfundisha, madaktari wanaomtibu yeye na watoto wake wanataabika kwa mshahara kiduchu.”

  Hata hivyo, pamoja na msimamo wake huo, Mzee Hongole hakuwa na maana ya kuwachukia wanasiasa, bali alikerwa na mfumo wetu wa namna inavyoonekana kutowajali ipasavyo, kwa maslahi, ‘of course’, wana-taaluma wenye kutoa mwanga wa maendeleo wakiwamo walimu, madaktari na watumishi wa kada nyingine muhimu.

  Mzee Hongole ambaye alipewa jina maarufu la - Njoo Uone- pamoja na kupigania maslahi kwa waandishi na wana-taaluma wengine, alikuwa na chuki kubwa kwa waandishi wavivu, wasiopenda kuuliza wanapokwama na wale waliokuwa wakifanya kazi kwa mazoea bila kubadilika kama wakati unavyosonga.

  Jina la Njoo Uone lilitokana na kuwa mhariri mkuu wa kwanza wa gazeti lenye jina hilo lililokuwa likimilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika ukanda wa Ubena (sasa ni mkoa mpya wa Njombe na maeneo mengine kukaribia Iringa) na Ulanga, Morogoro.

  Mbali na jina hilo, wapo waliomwita Mzee Kijana. Hawa ni wengi zaidi, tena wakiwa wa rika lake na aliowapita umri. Hili lilitokana na namna alivyokuwa akijipenda. Hakuwa mzee chafu, kwamba anavaa misurupwete, la hasha. Alipenda kuvaa nguo zake zikiwa zimekubali pasi, akitupia na koti juu lenye kuvutia.

  Kitu kikubwa ambacho naweza kukielezea ikiwa ni njia ya kumkumbuka 'Njoo Uone' ni namna ya pekee alivyopenda kufanya kazi na mimi. Sina uhakika ilikuwaje, kwani kwa muda mfupi sana, baada ya kuwa nimejiunga na magazeti ya Kwanza Jamii, alipenda kuniita na kukaa peke yetu na kunipa historia, kwanza ya vyombo vya habari maeneo ya kusini mwa Tanzania.

  Pia alipenda kunieleza kwamba lazima chombo chetu cha habari kiwe mfano wa kuigwa na vyombo vingine vikubwa; kwanza kwa kufuata maadili na kuzingatia matakwa ya wasomaji wetu. Hakusita kuniambia niwe mkali kwa kusimamia waandishi wasipende kuvaa nguo za ajabu ajabu- kwake hizo zilikuwa ni zile zinazobana, kuvaa suruali kwa waandishi wa wanawake na zaidi sana kuhakikisha gazeti linasambaa maeneo mengi ili lisomwe.

  Mzee Hongole amefariki wakati harakati za kuhakikisha magazeti yetu yanakuwa bora zaidi zinaendelea na wakati wa uhai wake amekuwa akishuhudia juhudi hizo na kutoa pongezi tunapofanya vyema bila kuuma uma maneno tunapokwenda mrama.

  Akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri ya Kwanza Jamii - Njombe, Mzee Hongole alikuwa mshauri muhimu katika kuboresha magazeti yetu akiunganisha mawazo na uzoefu wake na wajumbe wengine wote.

  Mbali na masuala ya magazeti na habari kwa jumla, Mzee Njoo Uone alikuwa mpiganaji kiongozi wa haki na maslahi kwa wakulima wa zao la chai, siyo Lupembe pekee, bali maeneo yote ya kusini mwa Tanzania.

  Kutokana na kutetea haki, wakulima wa chai wa maeneo hayo walimpa nafasi ya kuwa kiongozi wao kuwasemea, kuhakikisha wanapata maslahi mazuri kwa mazao yao na zaidi sana kuhakikisha chai inakuwa mkombozi wa wakulima wote na siyo kuwaneemesha matajiri tu- wengi wao wakiwa walanguzi wa kuwakandamiza wakulima.

  Nakumbuka, katika mazishi yake, wakulima wa chai, tena wadogo wadogo ndiyo walioongoza kwa kulia- siyo wanawake pekee, bali hata kina baba. Walitokwa machozi kumlilia mtetezi wao. Kumsindikiza mpiganaji wao na hakika wamepoteza jembe la kuongoza kupigania haki na maslahi yao.

  Ni vyema basi, wakati akiwa ametangulia huko, wengi wanakoamini kuwa ni mbele za haki, waandishi wa habari wakamuenzi Mzee Augustino Hongole, kwa kuwa waadilifu katika kazi zao na kuzingatia maadili ya taaluma yenyewe.

  Kila aliyefanya kazi na Njoo Uone, atakubaliana nami kuwa mwenzetu huyo alithamini na kuheshimu sana uwezo na kazi nzuri za wengine na alitoa pongezi zake kwa uwazi kwa kila kazi ya kupendeza iliyokuwa ikifanywa.

  Mzee Njoo Uone amefariki dunia baada ya kukumbwa na kasi ya ugonjwa wa kisukari na malaria akiwa katika Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam na kuzikwa kijijini kwake Isoliwaya.

  Ameacha mjane, watoto sita na wajukuu 17.

  Ewe Mzee Augustino Hongole. Ndugu yangu 'Njoo Uone.' Bosi wangu, pumzika kwa amani.

  *Mwandishi ni Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Kwanza Jamii