10 Feb 2012

Guest Post: Wabunge kufadhili miradi kunadumaza maendeleo

Richard Lucas
Guest post from Richard Lucas, Programme Manager of Daraja's Maji Matone programmeWabunge kufadhili miradi kunadumaza maendeleo 

Imekuwa jambo la kawaida kwa wananchi kuwaomba viongozi wao, hasa wabunge wawasaidie kugharamia miradi ya maendeleo. Mazoea haya yametufanya tusahau majukumu halisi ya wawakilishi wetu na pengine jukumu letu la kuwawajibisha pale wanapokwenda kinyume na wajibu wao.

Wabunge wamesahau majukumu yao ya msingi, badala yake wanajitwika majukumu ya serikali. Hali hii pia inasababisha wananchi tusahau vigezo muhimu vya kuchagua viongozi na kutumbukia kwenye mkumbo wa kuchagua viongozi matajiri-ambao nao wanaitumia fursa hiyo vilivyo kuimarisha utajiri wao pamoja na kuulinda.

Ieleweke kuwa sio wajibu wa wabunge kulipia/kugharamia miradi ya maendeleo majimboni mwao. Wabunge wengi wamekuwa wakitoa ufadhili mbalimbali katika majimbo yao, na kusahau majukumu yao ya msingi ya kuwawakilisha wananchi na kuwasilisha mawazo yao Bungeni ili yapatiwe ufumbuzi na kuisimamia, kuishauri na kuikosoa serikali katika kutoa huduma za jamii na kufanya miradi ya maendeleo.

Aidha, mfuko wa jimbo ambao, wabunge wa upinzania na chama tawala, CCM walisahau tofauti zao na kuupitisha kwa kishindo umekuwa nao ukitumika kama mali ya mbunge na katika kutafuta wema kwa wapigakura, wamekuwa wakiahidi mambo kadhaa huku wakiacha kuwaweka wazi wapigakura. Mwishowe wananchi wanaamini hizo ni huruma za mbunge wao.

Hali hii hakika umetupeleka pabaya kwani umesababisha na unaendelea kusababisha yafuatayo:

Mosi, hali ya wabunge kulipia miradi ya maendeleo kunavuruga utaratibu wa mchakato mzima wa mipango ya maendeleo. Tunazo sera nzuri za kusaidia jamii kuibua miradi ya maendeleo na fursa za hiyo miradi kuweza kugharamiwa. Hivyo wabunge wanapochukua jukumu la kugharamia miradi hiyo, kunafanya wananchi wanakosa imani/hawaoni umuhimu wa kufuata mchakato uliwekwa kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na badala yake wanatupia jukumu hilo kwa wabunge.

Pili, hali hii inapunguza uwajibikaji wa pande zote mbili hasa uwajibikaji wa wananchi. Mradi unaogharamiwa na wabunge, unakuwa mradi wa mbunge. Hivyo wananchi wanakosa umiliki wa miradi hii kitu ambacho kinafanya miradi hii isiwe endelevu, na zaidi isiwanufaishe wananchi kwa upana wake.

Wakati mbunge kwa upande wake anashindwa kutumia nafasi yake ya uwakilishi kwa kujenga hoja kwa lengo la kupata fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya wananchi. Hatima yake ni kwamba serikali haioni umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya wananchi kwani mbunge anazo hela na hataki ibainike kwamba serikali/wananchi wanaweza kuendeleza miradi yao wenyewe.

Pia, mwenendo huu wa wabunge husababisha migongano kwenye Serikali za Mitaa; hii hutokea  pale panapokuwepo fedha ambazo tayari zimeshatengwa kwa ajili ya miradi husika, ambapo fedha hizo zinaweza kuishia mikononi mwa wajanja. Wajibu wa mbunge katika hili ni kuwahamasisha wananchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi hii na kusimamia matumizi ya fedha ya miradi hii.

Tatu, wabunge kugharamia miradi ya maendeleo inachochea hali ya utegemezi ndani ya jamii zetu. Serikali kupitia sera ya ugatuzi wa madaraka inalenga kuijengea jamii utamaduni wa kujitegemea kwa kuitaka jamii ishiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama. Sasa mbunge anapofadhili hii miradi, inafanya wananchi wajijengee utamaduni wa kusubiri kufanyiwa kila kitu. Na ndiyo hali ilivyo sasa kwani mara nyingi wenye fedha ni rahisi kupata madaraka.

Nne, wananchi wanajikuta wanapima viongozi wao kwa ufadhili waliotoa badala ya kutathmini utekelezaji wa majukumu yao kama wabunge. Hii inasababisha watu wasiokuwa na uwezo wa kifedha kukosa nafasi za uongozi hata kama wanao uwezo wa kuongoza vizuri. Hali imesababisha wananchi wengi kukosa uwakilishi na kuongezeka kwa matatizo makubwa ya uongozi mbovu, ufisadi, rusha na hali ngumu ya maisha huku wachache wakiendelea kunufaika na rasilimali za nchi hii.  

Tano, wabunge wanaelemea katika kutafuta fedha za kugharamia miradi ya maendeleo badala ya kufanya majukumu yao ya msingi. Hii imesababisha wabunge kutoonekana majimboni kwa sababu inawabidi watafute mbinu mbalimbali za kupata fedha badala ya kutumia muda wao kutimiza majukumu yao ya msingi.

Badala ya kuwapigania wananchi ili kuwakwamua kutoka hali waliyonayo, wabunge wamejikuta wakipigania maslahi yao binafsi mfano wa sasa wa wanavyopambana kufa na kupona kuhalalisha kupanda kwa posho kwa madai ya kuwa wanatoa hela nyingi kwa wapiga kura kufadhili shughuli mbalimbali za maendeleo. Amenena mtu mmoja kuwa wanatumia fedha za walipa kodi kuwahonga wapiga kura.

Wewe una mtazamo gani kuhusu jambo hili na wajibu wa wabunge? Unafikiri mbunge kuwa na pesa nyingi kunaleta maendeleo endelevu? Tujadili, tuchukue hatua!