25 Jun 2012

Guest Post: Hotuba ya bajeti ya maji itoe majibu ya maswali haya

A guest post from Daraja's Richard Lucas, Programme Manager of the Maji Matone programme.


Hotuba ya bajeti ya maji itoe majibu ya maswali haya 
Katuni ya HabariLeo, tarehe 20 Juni, 2012

Mnamo tarehe 31, Mei 2012, kwenye gazeti la Mwananchi, mhariri alichapisha barua ya mwananchi wa kijiji cha Rungwa yenye kichwa cha habari ‘Waziri Mkuu tusaidie tupate maji’. Katika barua hii mwananchi huyu anamwomba Waziri Mkuu awasaidie kupata maji, maana kumekuwa na mkakati wa kuwaletea maji kwa miaka mingi ambao haujafanikiwa. Anaeleza kuwa mkakati huo ulikuwa ni wa kuwaletea mradi wa benki ya dunia ambapo walipaswa kuchanga asilimia tano ya gharama za mradi. Fedha hizo wameshazikamilisha miaka miwili iliyopita lakini hakuna kinachoendelea.

Kilio cha mwananchi huyu, ni kilio cha wananchi wengi katika kila wilaya. Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ilipanga kupatia vijiji kumi kila wilaya miradi ya maji. Washauri walichaguliwa, wakafanya tathmini, wakatengeneza michoro na kisha kuwahamasisha wananchi kujipanga na kuchangia asilimia kati ya 2.5 hadi 5 kutokana na aina ya mradi. Mchakato huu umekamilika takribani miaka mitatu iliyokwisha lakini miradi hii haitekelezwi.

Bajeti ya Maji

Mwaka wa fedha unaoisha (2011/12) serikali ilitenga bajeti ya sh 621.6 bilioni kwenye sekta ya maji ambapo katika hizo sh 86.7 bilioni zilielekezwa katika ujenzi wa miradi ya maji ya vijiji kumi kwenye serikali za mitaa. Sina uhakika kuwa fedha hizi zilitosha miradi kwenye vijiji vingapi, lakini Waziri mwenye dhamana anapaswa kutolea majibu swali hili kwenye hotuba ya bajeti ya maji. Pamoja na swali hili la msingi, tunataka Waziri atumie fursa hiyo kuwaeleza wananchi kinagaubaga hatima ya miradi ya vijiji kumi. Taarifa hizi ni muhimu kuwafikia wananchi kwa kuwa tayari wamekata tamaa, hawapo tayari kushirikiana na watendaji wa serikali kuhusu masuala ya maji.

Wakati bajeti ya nchi imeongezeka kufikia trilioni 15 kwa mwaka wa fedha 2012/13, serikali inakusudia kutenga sh 568.8 bilioni kwa ajili ya sekta ya maji, ambapo fedha hizo zimepungua kwa sh 52.8 toka bajeti inayokwisha. Bajeti hii inazidi kuwa pungufu zaidi endapo tutazingatia suala la mfumuko wa bei. Wazo hapa sio namna gani hii bajeti ni kidogo, bali ni namna gani bajeti hii imelenga kutatua kero za muda mrefu za maji. Ni vipaumbele gani ambavyo bajeti hii imelenga? Je malengo ya bajeti hii ndio matatizo ya makuu ya wananchi?

Changamoto ya usambazaji maji vijijini

Kutodumu kwa miundombinu ya maji ni changamoto kubwa katika jitihada za kuongeza upatikanaji maji safi na salama hasa vijijini. Kasi ya kuharibika kwa miradi ya maji inaweza kuwa sambamba na kasi yetu katika kujenga miradi mipya ya maji. Bajeti inayokuja ilenge kupambana na tatizo la kutodumu kwa miradi na miundombinu ya maji. Takwimu zinaonesha kuwa kwa miradi mipya, asilimia 25 inakuwa haifanyi kazi baada ya miaka miwili. Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo hili, ambazo zinahitaji kufanyiwa jitihada za dhati kupambana nazo.

Bajeti  ya maji izingatie nini

Mambo muhimu ya kuzingatia kwa sasa ni ufahamu na utekelezaji wa sera mpya ya maji (ya mwaka 2002) na sheria namba 12 ya mwaka 2009. Haya yafanyike kwa kuboresha mifumo pamoja na kuwajengea uwezo watumishi waweze kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika sera hizi. Zaidi juhudi za makusudi zifanyike kuwawezesha wananchi kufahamu taarifa za sera hizi, watambue majukumu yao ili waweze kuyatekeleza. Zaidi ya hapo inaonekana serikali inajenga miradi na kuitelekeza kwa wananchi.

Pia bajeti ilenge kuboresha uwezo halmashauri kufanya ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi ya maji inayoendeshwa na wananchi. Ufuatiliaji utawezesha halmashauri kutambua matatizo ya wananchi katika kuendesha miradi ya maji, na vile vile kuwawezesha kutimiza wajibu wao wa kusaidia na kushauri waendeshaji wa miradi ya maji vijijini. Miradi mingi inakumbwa na migogoro ambayo inasababisha miradi hiyo kuzorota na kufa. Halmashauri nyingi zinalalamika kutokuwa na rasilimali fedha na nyingine za kuwawezesha kusimamia na kushauri jamii katika uendeshaji wa miradi ya maji.

Jambo jingine ni uundwaji na usaijili wa vyombo vya watumia maji (COWSOs). Bajeti hii itenge fedha za kuwajengea uwezo wasajili walioteuliwa na halmashauri. Wasajili hawa wameteuliwa lakini hawafahamu vizuri sheria za maji, na hasa majukumu yao katika kusajili vyombo hivi. Pia, wahamasishaji wajengewe uwezo kuhusu sera, mipango, mikakati, sheria na mambo mengine muhimu yanayohusu maji ili waweze kuandaa wananchi kuunda vyombo thabiti vitakavyodumu. Tusipozingatia hili, miaka michache tutakuwa tunaongelea tatizo la kutodumu kwa vyombo hivi vya watumia maji (COWSO).

Haya ni baadhi ya mambo machache ya kimfumo ambayo yakifanyiwa kazi tunaweza kupiga hatua kubwa katika kutatua changamoto ya kutodumu kwa mifumo/miundombinu/miradi ya maji.

Tukumbuke kuwa wananchi wanahitaji maji na sio mikakati.Richard Lucas anapatikana kwa email kupitia richardlucas@daraja.org